- Author, Anne Soy & Peter Mwai
- Nafasi, BBC
ONYO: Makala hii ina maelezo ya ukatili, ambayo yanaweza kuwahuzunisha baadhi ya wasomaji.
Vifo vya makumi ya watu nchini Kenya kufuatia wimbi la maandamano huku polisi wakikabiliana na maandamano hayo, vilianza na mauji ya kupigwa risasi Rex Masai mwenye umri wa miaka 30.
Mauaji hayo yamezidi kuondoa imani ndogo iliyokuwepo kuhusu jukumu la polisi la kudumisha utulivu. Huku msururu mpya wa maandamano ukikaribia kuanza, kuna wasiwasi jinsi vikosi vya usalama vinavyoshughulikia maandamano hayo.
Tarehe 20 Juni ilikuwa siku ya pili ya maandamano dhidi ya mswada wa fedha ambao ungeongeza kodi mpya. Siku iliyotangulia haikuwa na matukio makubwa, lakini jua lilipotua siku ya Alhamisi, kila kitu kilibadilika katikati ya mji mkuu, Nairobi.
Waandamanaji walizidi kufanya maandamano. Maafisa wa polisi waliacha kutumia maji ya kuwasha na gesi ya kutoa machozi na kufyatua risasi za moto.
Masai alijikuta katikati ya vurugu hizo. Alipigwa risasi ya paja na kuvuja damu hadi kufa.
"Damu yake ilitapakaa mikononi mwangu," anasema rafiki yake, Ian Njuguna, ambaye alimkimbilia kujaribu ku*msaidia alipoanguka chini.
Wakati yeye na rafiki mwingine wakijaribu kumbeba kwenda nae hospitali ya karibu, anasema, “afisa alitupiga mabomu ya machozi [tulipokuwa] tumembeba rafiki yetu aliyekuwa anakaribia kufa."
"Tulikuwa tukizungumza naye kwa majonzi, tukimsihi asituache."
Takribani maafisa wanne wa polisi kufikia sasa wanakabiliwa na mashtaka ya kuwapiga risasi na kuwaua waandamanaji katika kipindi cha wiki nne zilizopita, huku kukiwa na miito ya kutaka haki itendeke kwa waathiriwa wa matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Maandamano Kenya: Jinsi bunge lilivyotenda kinyume na matarajio ya Wakenya
Maandamano Kenya 'yavamiwa na wahalifu'
Uchunguzi umekuwa mgumu
"Tunakosa ushirikiano kutoka kwa polisi na kwa kiwango fulani hata maafisa wetu wanapokea vitisho," anasema John Waiganjo, kamishna wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA).
Uchunguzi wa mauaji ya Masai bado haujafanikisha kuanza kwa mashtaka, wapelelezi wanakusanya ushahidi zaidi na kurekodi taarifa muhimu.
Waiganjo hakuzungumzia kisa hiki lakini alieleza, mamlaka yake inapochunguza majeruhi au kifo, inahitaji habari kuhusu mahali ambapo bunduki zilizohusika zilitoka na utambulisho wa maafisa wanaodaiwa kuhusika.
BBC imethibitisha video iliyorekodiwa wakati wa tukio na mahali ambapo Masai aliuawa, ikionyesha afisa wa polisi aliyevalia nguo za kawaida akifyatua risasi kwa umati wa waandamanaji waliokuwa wakikimbia kando ya barabara.
Njuguna anasema rafiki yake alituhumiwa isivyo sahihi na afisa aliyempiga risasi kwa sababu alikuwa na nywele msokoto.
“Alidhaniwa kuwa ameiba simu. Kulikuwa na duka lililoporwa. Kwa hiyo, walifikiri alikuwa mmoja wa waporaji, wakampiga risasi - kwa sababu gani? Kusokota nywele," ameiambia BBC, akiwa na hasira na kufadhaika.
Usiku aliouawa, familia ya Masai inasema daktari aliyetangaza kuwa amefariki, alithibitisha alipigwa risasi kwenye paja lake.
"Nilipofika [ambapo alifia], niliwaomba wahudumu wa afya kuufunua mwili wa mwanangu," mama yake, Gillian Munyao, aliiambia BBC siku moja baada ya tukio hilo. Aliona risasi ilipoingia kwenye paja lake.
Baada ya uchunguzi wa maiti, familia na marafiki wa Masai walishtuka kujua kwamba risasi haikukutwa mwilini mwake. Licha ya jeraha kuonekana upande mmoja tu na hakuna jeraha upande wa pili. Wanashuku kuwa ilitolewa.
BBC ilipomweleza Waiganjo kuhusu madai ya ushahidi kupotea, hakushangaa, kutokana na changamoto za IPOA za kukosa vifaa vya kusaidia uchunguzi wao.
Hilo linaweza kukwamisha jitihada za kutafuta haki licha ya mamlaka ya IPOA, kutaka taasisi zingine kutoa taarifa zozote muhimu.
BBC iliwasiliana na kaimu mkuu wa polisi Douglas Kiricho, ili ajibu tuhuma za kutatiza uchunguzi na kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.
Ingawa alikubali ombi hilo na kumwagiza msemaji wa polisi kujibu maswali yetu, hakuna jibu lililotolewa kufikia wakati wa kuchapisha makala hii licha ya kumkumbusha mara nyingi.
Mwenendo wa polisi
Haishangazi kusikia IPOA inasema imetatizika kupata mashahidi ili kurekodi taarifa kuhusu kesi ya Masai au nyinginezo, kwani mara nyingi watu wanaogopa kujitokeza.
IPOA inatumia taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mauaji, ukamataji kiholela na utekaji nyara ili kuanzisha uchunguzi.
BBC imepata makumi ya video ambazo zinaonyesha kile wanaharakati na IPOA, wanasema ni matumizi ya nguvu kupita kiasi na vurugu za polisi walipokuwa wakizima maandamano.
BBC imeweza kuthibitisha maeneo na muda wa matukio yaliyotokea kwa kutazama alama muhimu, zinazoweza kuonekana kwenye video na picha za Google Street View na ramani za satelaiti, ripoti za vyombo vya habari vya ndani na video zingine zinazoonyesha matukio hayo.
Video hizo ni pamoja na kuwafyatulia risasi waandamanaji wasio na silaha, kuwapiga kwa virungu, mashambulizi dhidi ya watu wanaotoa huduma ya kwanza, kushambuliwa kwa waandishi wa habari na kutekwa nyara.
Katika video moja iliyorekodiwa karibu na Bunge, muandamanaji anaonekana akiwaelekea polisi akiwa ameinua mikono yake juu. Muda mfupi baadaye, milio ya risasi inasikika.
Baadaye tunamwona akiwa amepakizwa nyuma ya gari la polisi, akiwa na majeraha kwenye miguu yote miwili, akipiga kelele.
"Sijafanya chochote, sijachoma gari lolote, wamenipiga risasi bure," anasema huku akionyesha majeraha kwenye miguu yake.
"Siyo haki kutumia risasi za moto au risasi za mpira kwa watu ambao hawana silaha," anasema Irungu Houghton, mkurugenzi mtendaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, tawi la Kenya.
Anasema kuna mfumo wa wazi wa kisheria wa utendaji kazi wa polisi nchini Kenya. "Huwezi kwenda zaidi ya ukurasa mmoja bila kusoma maneno juu ya haki za binadamu na huduma kwa raia."
“Badala ya kupunguza mvutano, au kuwezesha maandamano ya amani, tulichoona ni kujaribu kuzuia maandamano ya amani. Na hapo ndipo mambo yanapoharibika.”
"Ikiwa maandamano ni ya amani, polisi hawatakiwi kutumia vitoa machozi au maji ya kuwasha, au hata risasi za moto," anasema Waiganjo.
Jukumu lao ni kuwaongoza waandamanaji kwenye njia iliyokubaliwa, na "wanaweza tu kutumia bunduki pale maisha ya mtu yanapokuwa hatarini."
Alipoulizwa ikiwa anaamini haki itatendeka, mamake Masai alisema: “Unajua jinsi serikali inavyofanya kazi hapa, lakini acha niwe na matumaini mema.”
"Ninawaambia polisi, katika maandamano yanayokuja, wao ni wazazi kama sisi. Maumivu tunayohisi yanapaswa kuwa yao. Hatutalipiza kisasi. Tunamwachia Mungu.”
Kwa nini Wakenya bado wanaandamana?
Maandamano Kenya: Ukweli kuhusu farasi wa polisi walioibiwa, na habari nyingine za kupotosha
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi